Monday, May 24, 2021

Rais wa Mahakama ya Afrika afanya mazungumzo na Tume

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (wa pili kulia) na mgeni wake, Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Mhe. Jaji Sylvain Oré (wa pili kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Makamishna na viongozi wengine wa Tume, nje ya ofisi za THBUB Kanda ya Mashariki, Mtaa wa Luthuli Jijini Dar es Salaam, Mei 24, 2021. Wa kwanza kulia ni Kiongozi Mwandamizi wa Mahakama ya Afrika aliyeambatana na Mhe. Oré.
Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji mst.) akiongea wakati wa mazungumzo baina ya Ujumbe kutoka Mahakama ya Afrika na viongozi wa Tume. Mazungumzo hayo yalifanyika ofisi za THBUB Kanda ya Mashariki, Mtaa wa Luthuli Jijini Dar es Salaam, Mei 24, 2021.
Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Mhe. Jaji Sylvain Oré (kushoto) akimkabidhi zawadi Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji mst.) huku viongozi wengine wakishuhudia tukio hilo, Mei 24, 2021 ofisi za Tume, Mtaa wa Luthuli Jijini Dar es Salaam.
Akiwa mwenye uso wa furaha, Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji mst.) akifungua zawadi aliyopewa na mgeni wake huku viongozi wengine wakishangilia kwa makofi, Mei 24, 2021 ofisi za Tume, Mtaa wa Luthuli Jijini Dar es Salaam.
Na: Fadhili Muganyizi

MEI 24 mwaka huu, Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Mhe. Jaji Sylvain Oré alikutana na viongozi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) na kufanya mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali.

Mazungumzo hayo yalifanyika Ofisi za THBUB Kanda ya Mashariki zilizoko Mtaa wa Luthuli Jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo Rais huyo wa Mahakama ya Afrika aliijulisha Tume kuwa ziara yake ililenga kuonana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ili kujadiliana naye kuhusu Tanzania kujitoa kwenye Ibara ya 34(6) ya Itifaki ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu. Ibara hiyo inahusu nchi wanachama kushitakiwa na watu binafsi au Asasi za Kiraia mbele ya Mahakama ya Afrika.

Pia, Mhe. Oré aliwajulisha viongozi wa Tume kuhusu maadhimisho ya miaka 15 ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu yanayotarajiwa kufanyika Mwezi Novemba mwaka huu, na aliikaribisha Tume kushiriki katika maadhimisho hayo.

Akizungumzia kuhusu kuboresha ushirikiano baina ya Taasisi hizo mbili, Mhe. Oré aliahidi kuipatia Tume taarifa kuhusu matukio mbalimbali yatakayokuwa yanatokea katika Mahakama ya Afrika kupitia anuani ya barua pepe aliyopewa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume alimpongeza Mhe. Oré kwa juhudi kubwa anazofanya yeye na taasisi yake kuimarisha utawala wa sheria na haki za binadamu barani Afrika.

Aidha, alimshukuru kwa uamzi wake wa kuitembelea THBUB na kufanya mazungumzo ya pamoja, na aliahidi kwamba atahakikisha mashirikiano baina ya taasisi zao yanaimarishwa zaidi siku hadi siku.

No comments:

Post a Comment