Tuesday, August 17, 2021

THBUB na LHRC watiliana saini mkataba wa nyongeza wa mashirikano

Na Said Rashid

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) zimetiliana saini mkataba wa nyongeza (Adendum) wenye lengo la kuimarisha mashirikiano katika utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu, utawala wa sheria na utawala bora.

Tukio hilo lililofanyika mara baada ya kikao cha pamoja kilichofanyika makao makuu ya Ofisi za Tume, Jijini Dodoma leo (Agosti 17, 2021) limeshuhudiwa na viongozi na maafisa kutoka LHRC na THBUB, wakiwemo Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Anna Henga na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume, Bwana Nabor Assey ambao walitia saini nyaraka hizo kwa niaba ya taasisi zao.

Viongozi wengine walioshuhudia tukio hilo kutoka THBUB ni: Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji mstaafu), Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Mohamed Khamis, na Wahe. Makamishna wa Tume, Dkt. Fatma Khalfan, Dkt. Thomas Masanja, na Amina Talib Ally.

Kwa upande wa LHRC ni: Mkurugenzi wa Ujengaji Uwezo na Uwajibikaji, Bi. Felista Mauya, Afisa Programu ya Uchechemuzi, Bwana Raymond Kanegene, na Mkuu wa Ofisi ya LHRC Dodoma, Bwana William Mtwazi.

Mkataba huo wa nyongeza wa mashirikiano umeainisha maeneo manne (4) makuu ya mashirikiano, ambayo ni: Uanzishaji na uwezeshaji utekelezaji wa shughuli zinazolenga kulinda na kukuza haki za makundi maalumu ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu na ubadilishanaji uzoefu na utaalamu katika michakato mbalimbali ikiwemo utayarishaji na uthibitishaji wa taarifa, uwasilishaji na usambazaji wa mapendekezo ya Universal Periodic Review (UPR) kwa umma.

Maeneo mengine ni: Ushirikiano katika shughuli za kuwajengea uwezo katika masuala ya haki za binadamu na utawala bora Viongozi wa Serikali za Mitaa, hususan Wakuu wa Wilaya na Madiwani na kuanzisha, kufuatilia na kuimarisha Klabu za haki za binadamu katika taasisi za elimu kuanzia ngazi ya Msingi hadi Chuo Kikuu.

Tume na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu zilitiliana saini mkataba wa awali wa mashirikiano katika utoaji wa elimu kwa umma na ufuatiliaji wa masuala ya haki za binadamu nchini mwaka 2018.


Kaimu Katibu Mtendaji wa THBUB, Bwana Nabor Assey na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Bi. Anna Henga wakitia saini Mkataba wa nyongeza mashirikiano katika maeneo maalumu ya ukuzaji na ulinzi wa haki za binadamu nchini. Hafla hiyo fupi ya utiaji saini ilifanyika mara baada kikao baina ya THBUB na LHRC kilichofanyika makao Makuu ya ofisi za Tume, jijini Dodoma leo (Agosti 17, 2021).
Kaimu Katibu Mtendaji wa THBUB, Bwana Nabor Assey na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Bi. Anna Henga wakibadilishana nyaraka mara baada ya kutia saini leo (Agosti 17, 2021).
Kaimu Katibu Mtendaji wa THBUB, Bwana Nabor Assey na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Bi. Anna Henga wakionyesha mkataba wa nyongeza wa mashirikiano mara baada ya kutia saini leo (Agosti 17, 2021) makao Makuu ya ofisi za Tume, jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji Mst.) akisikiliza kwa umakini mchango wa mmoja wa washiriki wa kikao baina ya THBUB na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilichofanyika leo (Agosti 17, 2021) makao Makuu ya Ofisi za Tume zilizoko Kilimani, jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Bi. Anna Henga akieleza jambo kwenye kikao baina ya THBUB na LHRC kilichofanyika leo (Agosti 17, 2021) makao Makuu ya Ofisi za Tume, jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wa kikao baina ya THBUB na LHRC wakiendelea na mazungumzo makao Makuu ya ofisi za Tume, jijini Dodoma leo (Agosti 17, 2021).
Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (katika) na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Bi. Anna Henga (wa pili kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka LHRC na viongozi wa Tume mara baada ya kuhitimisha kikao cha pamoja kilichofanyika leo (Agosti 17, 2021) makao makuu ya Ofisi za Tume, jijini Dodoma.

(Picha zote na Susan Ndashuka)

No comments:

Post a Comment