Na Germanus Joseph
ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bwana Francis Nzuki ameishauri Tume kurejesha ziara za vijijini zilizokuwa zimesimama kutokana na ufinyu wa bajeti. Kiongozi huyo mstaafu pia amewaasa watumishi wa Tume kuwajibika ipasavyo katika kazi. Bwana Nzuki ametoa ushauri huo hivi karibuni (Aprili 13, 2021) katika hafla fupi ya kuwaaga watumishi sita (6) wa Tume ambao utumishi wao ulikoma kisheria kwa nyakati tofauti. Akizungumza katika hafla hiyo Bwana Nzuki alisema: “Naipongeza Tume na Menejimenti kwa kazi nzuri, na hususan kwa jitihada za Tume zilizopelekea ukomo wa bajeti (budget ceiling) kuongezeka.” Mstaafu huyo aliongeza kuwa: “Ikiwa bajeti imeongezeka, ningeshauri kazi ya ziara za vijijini iliyokuwa inaachwa kila wakati kutokana na ufinyu wa bajeti irejeshwe.” Kwa maoni yake kazi hiyo ni muhimu kwa sababu siyo tu inachangia kuongeza uelewa wa umma, bali pia Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi hupenda kujua hatua ambayo Tume imefikia katika kueneza elimu ya haki za binadamu na utawala bora nchini. Akizungumzia uwajibikaji katika kazi Bwana Nzuki alisema: “Ningependa kuwaasa... wakati unafanya kazi uwe committed, fanya kazi kwa umakini, mwajiri atakutambua...tulia kwenye mafaili, utaona siku zinavyoenda unazidi kuthaminiwa.” Aidha, aliwataka watumishi hao wajitume kwa kuwa Tume inawatarajia wao waweze kuibadilisha. Vilevile Mkurugenzi huyo mstaafu aliiomba Tume kufanya uchechemuzi kwa kutumia potifolio za bunge ili kamati ya haki za binadamu na utawala bora ianzishwe bungeni. Kiongozi huyo anaamini kuwa uwepo wa kamati hiyo utayapa nguvu masuala ya haki za binadamu na utawala bora hapa nchini. Bwana Nzuki ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Haki za Binadamu ni miongoni mwa watumishi wachache kuitumikia Tume kwa muda mrefu; hadi anastaafu mwaka 2020 alikuwa ameitumikia taasisi hiyo kwa muda wa miaka 40. Watumishi wengine walioagwa katika hafla hiyo ni: Bwana Peter Massawe; Bi. Saida Kijangwa; Bwana Abdallah Abdallah; Bwana Dhamir Juma na Bwana Issa Kibito, ambaye hakuweza kuhudhuria hafla hiyo kwa sababu zisizozuilika.Tuesday, April 13, 2021
Tume yashauriwa kurejesha ziara vijijini
Bwana Francis Nzuki (mstaafu) akitoa nasaha zake kwa watumishi wa THBUB wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wastaafu iliyofanyika makao makuu ya ofisi za Tume, Kilimani Jijini Dodoma Aprili 13, 2021.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bwana Nabor Assey akitoa neno wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wastaafu wa Tume iliyofanyika makao makuu ya ofisi za Tume mtaa wa Kilimani Jijini Dodoma Aprili 13 mwaka huu.
Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Mohammed Khamis (kushoto) akimkabidhi Bwana Dhamir Juma zawadi na cheti cha kutambua utumishi wake kwa umma wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wastaafu hao Aprili 13, 2021. Katikati ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume, Bwana Nabor Assey akishuhudia tukio hilo.
Mtumishi wa Tume, Bi. Susan Ndashuka akiwamiminia wastaafu kinywaji (Shampeni) wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wastaafu hao iliyofanyika Aprili 13, mwaka huu makao makuu ya ofisi za Tume, Kilimani Jijini Dodoma.
Wakati wa kumtaja ‘Chales’ ulifika. Pichani wastaafu, Bwana Abdallah Abdallah na Bi. Saida Kijangwa wakiwa wameweka glasi zao tayari tayari kwa ajili ya kugonga cheers na viongozi na watumishi wa Tume ili kutakiana kheri na afya njema Aprili 13, 2021
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (wa tatu kulia) pamoja na Makamishna (mstari wa nyuma) wakiwa katika picha ya pamoja na wastaafu wa Tume muda mfupi kabla ya hafla ya kuwaaga. Kutoka kushoto ni: Bwana Dhamir Juma, Bwana Francis Nzuki, Bi. Saida Kijangwa, Bwana Peter Massawe na Bwana Abdallah Abdallah. Hafla hiyo ilifanyika hivi karibuni makao makuu ya ofisi za Tume, Kilimani Jijini Dodoma. (Picha zote na Suzan Ndashuka)
No comments:
Post a Comment