Na Germanus Joseph
MSTAAFU wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bi. Saida Kijangwa hivi karibuni amewataka watumishi wanawake wa Tume kushikamana na kufanya kazi kwa bidii ili wasimwangushe Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Akiongea katika hafla fupi ya kuwaaga watumishi wastaafu wa Tume iliyofanyika makao makuu ya ofisi za THBUB, Kilimani Jijini Dodoma, Bi. Saida alisema: “Akina mama tuache mambo ya hapa na pale, tushikamane, tushikamane akina mama, tufanye kazi akina mama...tusimwangushe yule mama.”
“Naamini historia yake (Mama Samia) tumeisikia...alianzia ukarani masijala...,” Bi. Saida alisema, na kuongeza: “Kwa hiyo tufanye kazi ili yule mama awe na imani na akina mama...akina mama tunaweza!”
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Mohammed Khamis aliwashukuru wastaafu waliokuwa wanaagwa kwa utumishi wao uliotukuka, nasaha zao, na kwa kuhudhuria hafla hiyo.
“Nyote mlikuwa mme-settle huko na mlikuwa mnashughulika na mambo mengine, lakini mmeacha shughuli zenu mkasema mjumuike nasi, ni heshima kubwa kwetu, asanteni sana,” alisema.
Pia kiongozi huyo alisema kuwa watumishi wa Tume wana mengi ya kujifunza kutoka kwa wastaafu hao kutokana na utendaji wao wa kazi, uzalendo na mienendo yao walipokuwa kazini.
“Tunaahidi kuzichukua nasaha zenu zote na kuzifanyia kazi,” Mhe. Mohammed Khamis alisema, na kuongeza “tutakapowahitaji mtusaidie jambo lolote msituchoke.”
Katika hafla hiyo iliyofanyika Aprili 13 mwaka huu wastaafu hao walitunukiwa vyeti vya kutambua utumishi wao na zawadi mbalimbali
No comments:
Post a Comment