Na Germanus Joseph
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binirith Mahenge ameitaka mifuko ya hifadhi ya jamii nchini kutoa mafao ya wastaafu kwa wakati ili kuondokana na kero iliyopo.
Kiongozi huyo pia amewaagiza waajiri nchini kuhakikisha kuwa mabaraza ya wafanyakazi yanaanzishwa katika sehemu zao za kazi.
Dkt. Mahenge ametoa wito huo leo (Mei 1, 2021) jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kimkoa uwanja wa Jamhuri jijini humo. Maadhimisho hayo yalibeba kauli mbiu isemayo: “Maslahi bora, Mishahara Juu – Kazi iendelee.”
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo ucheleweshwaji wa stahiki za wastaafu hivi sasa imekuwa changamoto kubwa na limekuwa suala linalolalamikiwa mno.
Hivyo, amewataka viongozi na watendaji ndani ya mifuko ya hifadhi ya kijamii kuhakikisha kero ya ucheleweshwaji wa mafao ya watumishi waliostaafu inamalizwa haraka.
Akizungumzia mabaraza ya wafanyakazi, kiongozi huyo alisema kuwa uanzishwaji wa mabaraza hayo ni takwa la kisheria, kwa hali hiyo aliwataka waajiri ambao bado hawajayaanzisha wayaanzishe mara moja.
Mapema akizungumza katika maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) mkoani Dodoma, Lizz Msechu aliiomba Serikali kuona uwezekano wa kuongeza mishahara ili kuwapa wafanyakazi unafuu wa maisha.
Pia aliiomba Serikali kuwapunguzia wafanyakazi mzigo wa kodi kwa kulipa mara moja tofauti na ilivyo sasa ambapo wanalipishwa mara mbili – kwa kukatwa kwenye mishahara yao, na wanaponunua bidhaa na huduma mbalimbali.
Vilevile kiongozi huyo alizungumzia ucheleweshwaji wa mafao ya wastaafu na baadhi ya waajiri kutoruhusu uanzishishwaji wa mabaraza ya wafanyakazi katika sehemu zao za kazi.
No comments:
Post a Comment