MWENYEKITI wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji Mst.) amewataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Tume kuwakumbusha watumishi wenzao kutekeleza majukumu ya taasisi kikamilifu.
Pia ameushauri uongozi wa Tume kushirikiana kwa karibu na uongozi wa Baraza la Wafanyakazi la Tume na Chama cha Wafanyakazi (TUGHE) tawi la THBUB katika kutatua kero za watumishi ili kuleta ufanisi kiutendaji.
Mhe. Mwaimu ameyasema hayo Februari 21, 2022 wakati akifungua mkutano wa 20 wa Baraza la Wafanyakazi wa THBUB uliofanyika kituo cha mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma. Mhe. Mwenyekiti aliwaambia wajumbe wa Baraza kuwa “nyie ni wawakilishi wa watumishi wengine, tuwakumbushe watumishi wenzetu kutekeleza majukumu ya Tume kikamilifu, kwa kuwa ndiyo tutapimwa nayo.”
Aidha, alihimiza kuhusu ushirikiano baina ya uongozi wa Tume, Baraza la Wafanyakazi, na Chama cha Wafanyakazi kuwa utasaidia katika kuendelea kuwakumbusha wajumbe wa Baraza wajibu wao, kushughulikia maslahi ya watumishi na katika utoaji huduma za taasisi.
Mhe. Jaji Mstaafu alitumia fursa hiyo pia kuwapongeza viongozi na wajumbe wa Baraza kwa kuchaguliwa kwao kuwawakilisha watumishi wenzao katika Baraza hilo. Pia aliwataka kuzitumia nyadhifa walizokasimiwa kwa manufaa ya Baraza, taasisi na watumishi wenzao.
Awali kikao hicho kilianza kwa kufanya uchaguzi wa Katibu na Katibu Msaidizi wa Baraza hilo kwa miaka mitatu ijayo. Waliochaguliwa kushika nafasi hizo ni: Maafisa Wachunguzi Wakuu Bwana Emmanuel Ndosi (Katibu) na Bi. Jovina Muchunguzi (Katibu Msaidizi).
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Baraza, mmoja wa wajumbe, Bwana Yohana Mcharo aliishukuru Serikali kwa kuanzisha mabaraza ya Wafanyakazi sehemu za kazi, ambapo kwa asilimia kubwa yanasaidia kufikisha ushauri, maoni na changamoto za watumishi kwa menejimenti za taasisi.
Uwepo wa mabaraza ya Wafanyakazi husaidia kuweka uwazi, usawa na demokrasia ambayo husaidia kuleta ufanisi,” alisema Bwana Mcharo. "
Katika mkutano huo uliowashirikisha takriban wajumbe 60 kutoka makao makuu ya Ofisi za Tume Dodoma, Ofisi ya Tume Zanzibar na Ofisi za Tume za matawi ya Dar es Salaam, Lindi, Pemba na Mwanza, washiriki walijifunza majukumu yao.
Pia, walipokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya Julai - Desemba, 2021, Taarifa ya Makadirio ya Bajeti ya Mwaka ujao wa fedha (2022/2023), Taarifa ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu na Hoja za TUGHE.
No comments:
Post a Comment