Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji Mstaafu) amesema hivi karibuni taasisi yake itafanya ufuatiliaji kuhusu utekelezaji wa haki za wafanyakazi na viwango vya ajira katika makampuni binafsi ya ulinzi.
Akiongea na vyombo vya habari Makao Makuu ya Tume, Kilimani jijini Dodoma leo Februari 2, 2024 Mhe. Mwaimu amesema kuwa ufuatiliaji huo utafanyika kuanzia Februari 5 hadi 10, 2024 katika mikoa ya Iringa, Dar es Salaam na Kagera.
“Kazi hii inalenga kufuatilia utekelezaji wa Sheria na Kanuni zinazoyataka makampuni ya aina zote kutekeleza majukumu yao kwa kuheshimu haki za binadamu na upatikanaji wa suluhisho na fidia kwa wahanga wa ukiukwaji wa haki za binadamu unaohusishwa na shughuli za kibiashara au uwekezaji,” Mhe. Jaji Mstaafu amesema.
Ameongeza kuwa miongoni mwa maeneo yatakayoangaliwa katika ufuatiliaji huo ni pamoja na: Mikataba ya ajira, iwapo inakidhi viwango vya ajira; afya na usalama kazini; na utunzaji wa taarifa binafsi za waajiriwa.
Maeneo mengine ni: Uwepo wa vyama vya wafanyakazi; mahusiano ya makampuni ya ulinzi na jamii; na stahili nyingine wanazopaswa waajiri kutoa kwa wafanyakazi wao.
Aidha, Mhe. Mwaimu amesema kuwa baada ya ufuatiliaji huo, Tume itatoa taarifa yenye mapendekezo ya namna ya kuboresha uzingatiaji wa haki za wafanyakazi na viwango vya ajira katika makampuni binafsi ya ulinzi.
Utekelezaji wa kazi hii ni mwendelezo wa ufuatiliaji wa masuala ya biashara na haki za binadamu nchini, Mhe. Mwenyekiti amesema, na kuongeza kuwa Mwezi Desemba 2023 Tume ilifanya tathimini ya utendaji kazi kwa taasisi zisizo za kimahakama zinazoshughulikia malalamiko na migogoro inayohusiana na masuala ya biashara na haki za binadamu.
“Tume inatoa shukrani zake za dhati kwa Serikali kwa kuipatia mazingira wezeshi kutekeleza majukumu yake, na kwa Taasisi ya Haki za Binadamu nchini Denmark (Danish Institute for Human Rights - DIHR) kwa kuiwezesha kiufundi na kirasilimali kufanikisha utekelezaji wa kazi hii na nyingine zilizotangulia.



No comments:
Post a Comment