Wednesday, March 13, 2024

Mamlaka zatakiwa kutekeleza mapendekezo ya THBUB kwa wakati

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wawakilishi wa Taasisi za Serikali na Maafisa wa Tume mara baada ya kufungua mkutano wa siku moja wa kujadili utekelezaji wa mapendekezo ya Tume uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma leo Machi 13, 2024.
Leo Machi 13, 2024, Ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Mkoa jijini Dodoma: Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji Mstaafu) akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano baina ya Tume na taasisi za Serikali kuhusu utekelezaji wa mapendekezo ya Tume yaliyotokana na chunguzi za malalamiko ya wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi nchini.
Wawakilishi wa Taasisi za Serikali na Maafisa wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wakijadili utekelezaji wa mapendekezo ya Tume leo Machi 13, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Mwakilishi wa Taasisi mojawapo ya Serikali akizungumza wakati wa mkutano baina ya THBUB na Taasisi za Serikali wakati wa kujadili utekelezaji wa mapendekezo ya Tume yaliyotokana na chunguzi za malalamiko ya wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi nchini, uliofanyika leo Machi 13, 2024 ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Mkoa jijini Dodoma.
Mwakilishi wa Taasisi mojawapo ya Serikali akizungumza wakati wa mkutano baina ya THBUB na Taasisi za Serikali wakati wa kujadili utekelezaji wa mapendekezo ya Tume yaliyotokana na chunguzi za malalamiko ya wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi nchini, uliofanyika leo Machi 13, 2024 ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Mkoa jijini Dodoma


Wito umetolewa kwa mamlaka mbalimbali zinazopokea mapendekezo ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kutekeleza mapendekezo hayo kwa wakati na kutoa mrejesho.

Wito huo umetolewa leo Machi 13, 2024 na Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji Mstaafu) alipokuwa akifungua mkutano wa siku moja baina ya Tume na wawakilishi wa mamlaka za Serikali uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa jijini Dodoma.

Wawakilishi hao walikutana kwa ajili ya kujadili utekelezaji wa mapendekezo ya Tume yaliyotokana na chunguzi kadhaa za malalamiko ya wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi.

Katika hotuba yake ya ufunguzi Mheshimiwa Mwaimu aliwaeleza wajumbe wa mkutano kuwa taasisi yake ilifikia uamuzi wa kukutana na mamlaka hizo kutokana na mwitikio mdogo katika utekelezaji wa mapendekezo yake.

“THBUB imeona kuna haja ya kukutana pamoja na kujadili hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa kwa taasisi zenu," Mheshimiwa Mwaimu alisema, na kuongeza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

Kulingana na Mheshimiwa Mwenyekiti Tume inao wajibu wa kufuatilia mapendekezo yake katika mamlaka husika kwa kuwasiliana na mamlaka hizo kwa njia mbalimbali, ikiwemo barua, simu, kukutana ana kwa ana na watendaji wa mamlaka hizo kwa kufika katika ofisi zao na katika mkutano kama huo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Wawakilishi kutoka Halmashauri ya Mji wa Muheza, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, TAKUKURU, na Jeshi la Polisi.

Wajumbe wengine walitoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara Mambo ya Ndani ya Nchi, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), na Ofisi ya Waziri Mkuu


Tuesday, March 12, 2024

Mashirika yasiyo ya kiserikali ya IGT na BASIS yatembelea Tume

Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Thomas Masanja (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi waandamizi wa Shirika la BASIS International Limited la nchini Uganda na Shirika la Kukuza Utawala Bora na Uwazi Tanzania (Intiative for Good Governance and Transparance – IGT) la jijini Mwanza, mashirika hayo yalipotembelea Makao Makuu ya Ofisi za Tume zilizopo Kilimani jijini Dodoma leo Machi 12, 2024.


Mashirika mawili yasiyo ya kiserikali yanayojishughulisha na ukuzaji wa uwajibikaji, kwa pamoja leo Machi 12, 2024 yametembelea Makao Makuu ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) jijini Dodoma na kufanya mazungumzo na uongozi wa juu wa Tume.

Katika mazungumzo yao, Tume na mashirika hayo mawili, BASIS International Limited la nchini Uganda na Shirika la Kukuza Utawala Bora na Uwazi Tanzania (Intiative for Good Governance and Transparance – IGT) lenye makao yake jijini Mwanza wametafakari kuhusu kuwa na mashirikiano katika ukuzaji na ulinzi wa haki za binadamu katika jamii zilizopo pembezoni mwa maeneo zinakofanyika shughuli za migodi.

Akiongea wakati wa mazungumzo hayo, Kamishna wa THBUB, Dkt. Thomas Masanja aliueleza ugeni huo kuwa Tume imefurahishwa na ujio wao, na kwamba taasisi yake iko tayari kufanya kazi nao.

Mkurugenzi wa IGT, Bwana Edwin Soko aliongoza Ujumbe wa taasisi hizo katika ziara hiyo akiambatana na maafisa wake wawili, Bi. Frida Mwenda (Afisa Programu) na Bi. Catherine Masanja (Afisa wa masuala ya Jinsia).

Wengine katika Ujumbe huo kutoka BASIS International Limited walikuwa Bwana Tony Binyina (Meneja Miradi) na Bwana Michael Moasa (Meneja TEHAMA).


Friday, March 8, 2024

THBUB yapamba maadhimisho ya siku ya Wanawake 2024

Watumishi Wanawake wa Ofisi ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora tawi la Dar es Salaam wakiwa katika picha ya pamoja muda mfupi kabla ya kuungana na Wanawake wenzao katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake yaliyofanyika kimkoa viwanja vya Mji Mwema wilayani Kigamboni, leo Machi 8, 2024.
Baadhi ya Watumishi Wanawake wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Ofisi Kuu Dodoma wakifuatilia hotuba wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake yaliyofanyika kimkoa viwanja vya Shule ya Msingi Chinangali wilayani Chamwino leo Machi 8, 2024.
Baadhi ya Watumishi Wanawake wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Ofisi Kuu Dodoma wakifuatilia hotuba wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake yaliyofanyika kimkoa viwanja vya Shule ya Msingi Chinangali wilayani Chamwino leo Machi 8, 2024.
Baadhi ya Watumishi Wanawake wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Ofisi Kuu Dodoma wakiandamana wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake yaliyofanyika kimkoa viwanja vya Shule ya Msingi Chinangali wilayani Chamwino leo Machi 8, 2024.
Watumishi Wanawake wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Ofisi Kuu Dodoma wakiwa katika picha ya pamoja huko Chamwino muda mfupi kabla ya kuanza kwa maandamano wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake yaliyofanyika kimkoa viwanja vya Shule ya Msingi Chinangali wilayani Chamwino, leo Machi 8, 2024.
Watumishi Wanawake wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Ofisi Kuu Dodoma wakiwa katika picha ya pamoja huko Chamwino muda mfupi kabla ya kuanza kwa maandamano wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake yaliyofanyika kimkoa viwanja vya Shule ya Msingi Chinangali wilayani Chamwino, leo Machi 8, 2024.
Watumishi Wanawake wa Ofisi ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora tawi la Mwanza wakiwa katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake yaliyofanyika kimkoa wilayani Misungwi, leo Machi 8, 2024. Wa kwanza kulia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi, Bi. Angela Mshana, alienda huko kikazi.
Baadhi ya Watumishi Wanawake wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Ofisi Kuu Dodoma wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuwasili huko Chamwino leo Machi 8, 2024. Aliyevaa ushungi na miwani (katikati) ni Kamishna wa THBUB, Mhe. Amina Talib Ali aliyewaongoza Wanawake hao katika maadhimisho hayo.
Kamishna wa THBUB na Msimamizi wa masuala ya Makundi Maalum, Mhe. Amina Talib Ali.


Leo Machi 8, 2024 Watumishi Wanawake wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wameungana na wanawake wenzao nchini kote kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake iliyobeba Kauli mbiu isemayo: “Wekeza kwa Wanawake kuharakisha maendeleo ya Taifa na ustawi wa jamii.”

Hakika ushiriki wao uliifanya siku hiyo kuwa ya kupendeza kutokana na mavazi mazuri na ya aina yake waliyoyavaa. Itoshe kusema, ‘pamba’ walizopiga zilivutia macho ya kila aliyewatazama – walipendeza!

Kamishna wa THBUB na Msimamizi wa masuala ya Makundi Maalum, Mhe. Amina Talib Ali aliwaongoza Wanawake hao katika maadhimisho hayo mkoani Dodoma, ambako kimkoa yalifanyika viwanja vya Shule ya Msingi Chinangali wilayani Chamwino.

Uwepo wa THBUB pia ulionekana katika maadhimisho yaliyofanyika katika majiji ya Dar es Salaam na Mwanza ambako Tume inazo Ofisi zake za matawi.

Hii ni mara ya 27 Taifa letu linaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake iliyoridhiwa na Umoja wa Mataifa na kuanza kuadhimishwa kwingine duniani mwaka 1975.


THBUB yaipongeza Serikali kwa kuendeleza haki za Wanawake

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Khamis Hamad.
Baadhi ya Watumishi Wanawake wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wakifuatilia hotuba wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake yaliyofanyika kimkoa viwanja vya Shule ya Msingi Chinangali wilayani Chamwino, Dodoma leo Machi 8, 2024.
Baadhi ya Watumishi Wanawake wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wakifuatilia hotuba wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake yaliyofanyika kimkoa viwanja vya Shule ya Msingi Chinangali wilayani Chamwino, Dodoma leo Machi 8, 2024.
Baadhi ya Watumishi Wanawake wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) wakiwa katika maandamano wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa Wanawake yaliyofanyika kimkoa viwanja vya Shule ya Msingi Chinangali wilayani Chamwino, Dodoma leo Machi 8, 2024.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imezipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa kutekeleza haki na utu wa mwanamke nchini.

Imezitaja hatua hiyo kuwa ni pamoja na kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi na ajira, kuhakikisha usawa wa kijinsia kati ya wanawake na wanaume, na kupambana na ukatili wa kijinsia na mila kandamizi.

Hayo yameelezwa kwenye taarifa iliyotolewa jijini Dodoma na Makamu Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Mohamed Khamis Hamad leo Machi 8, 2024 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake.

Pamoja na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali, taarifa hiyo imeeleza kuwa bado zipo changamoto kadhaa zinazowakabili Wanawake hapa nchini.

Imezitaja changamoto hizo kuwa ni uchache wa Wanawake katika nafasi za ajira na uongozi, uwepo wa vitendo vya ukatili wa kijinsia, uwepo wa mila na desturi kandamizi, Wanawake wenyewe kushindwa kuthubutu na kujiamini katika kuwania nafasi za uongozi, umasikini, na ushirikishwaji duni katika kufanya maamuzi kuanzia ngazi ya familia.

Kutokana na changamoto hizo, Tume  inapendekeza kuwa Serikali itekeleze mikataba yote ambayo nchi imeridhia, taarifa hiyo imeeleza.

Pia, inapendekeza kuwa Serikali zote mbili, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi Zanzibar, kuendelea kuongeza ushiriki wa Wanawake katika uwekezaji na biashara ili kuchochea maendeleo ya Taifa na jamii kwa ujumla.

Vilevile, Tume imetoa wito kwa Asasi za kiraia, mashirika ya Kidini na wadau wengine kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuondokana na mila kandamizi zinazochangia Wanawake kubaki nyuma kimaendeleo.

Mkoani Dodoma maadhimisho hayo yamefanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Chinangali Wilayani Chamwino na yameongozwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maaulum, Mhe. Dorothy Gwajima akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kasim Majaliwa kama Mgeni Rasmi.


Thursday, February 15, 2024

Jaji Mwaimu alitaka Baraza la wafanyakazi THBUB kutoa elimu kuhusu wajibu

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la THBUB na wageni waalikwa mara baada ya kufungua mkutano wa 22 wa Baraza hilo uliofanyika kituo cha mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC) jijini Dodoma leo Februari 15, 2024. Kulia kwa Mhe. Mwenyekiti ni Katibu Mtendaji wa Tume, Bwana Patience Ntwina, na kushoto kwake ni Naibu Katibu Mtendaji wa Tume, Bwana Juma Karibona. Wengine (waliokaa) ni Katibu wa Baraza, Bwana Emmanuel Ndosi (mwenye miwani) na Katibu Msaidizi wa Baraza, Bi. Jovina Muchunguzi.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji Mstaafu) akitoa hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa siku moja wa Baraza la Wafanyakazi la THBUB kituo cha mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC) jijini Dodoma leo Februari 15, 2024.
Baadhi ya wajumbe na wageni waalikwa wakifuatilia wasilisho lililokuwa likitolewa wakati wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la THBUB kituo cha mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC) jijini Dodoma leo Februari 15, 2024.
Wajumbe wa Baraza, Bi. Bitizani Kejo (mwenye ushungi) kutoka Ofisi ya Tawi Dar es Salaam na Bi. Eugenia Lohay kutoka Idara ya Huduma za Kisheria Makao Makuu ya Tume Dodoma wakifuatilia mjadala wakati wa mkutano wa 22 wa Baraza la Wafanyakazi la THBUB kituo cha mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC) jijini Dodoma leo Februari 15, 2024.
Mjumbe mwalikwa, Mkurugenzi Msaidizi (Utawala Bora), Mbwana Mussa Mbwana akichangia hoja wakati wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la THBUB kituo cha mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC) jijini Dodoma leo Februari 15, 2024. Wengine kutoka kulia ni Afisa Mfawidhi Ofisi ya Tume tawi la Dar es Salaam, Bi. Shoma Phillip, Afisa Mfawidhi Ofisi ya Tume Zanzibar, Bi. Saada Masoud na Mkurugenzi Msaidizi (Utafiti na Nyaraka), Bi. Fides Shao.


Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji Mst.) amewataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Tume kuwaelimisha watumishi wenzao na wananchi kutimiza wajibu wao.

Pia, aliishauri Menejimenti ya Tume kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wasiotekeleza wajibu wao, kutoa kipaumbele katika kushughulikia changamoto za watumishi, na kuandaa mpango endelevu wa mafunzo.

Mhe. Mwaimu ameyasema hayo leo Februari 15, 2024 wakati akifungua mkutano wa 22 wa Baraza la Wafanyakazi la THBUB uliofanyika kituo cha mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC) jijini Dodoma.

“Kwa vyovyote vile hakuna haki bila wajibu, kwa hiyo tuna kazi kubwa kuhakikisha kuwa ... wanaohitaji haki tunawasaidia na kuwaelimisha kuhusu wajibu wao wa kufuata sheria na taratibu za kupata haki,” Mhe. Mwenyekiti aliwaambia wajumbe wa Baraza, “huu wajibu ni kwa ... watumishi na ... wadau wetu.”

Kwa mujibu wa Mheshimiwa Jaji Mstaafu Mwaimu Menejimenti inapochukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wasiowajibika ipasavyo husaidia kuhakikisha majukumu ya taasisi husika yanatekelezwa kikamilifu kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa.

Akizungumzia changamoto za watumishi, Mheshimiwa Mwenyekiti alibainisha kuwa changamoto hizo ni pamoja na malimbikizo ya mishahara, madai ya likizo, kupandishwa vyeo, na maslahi bora.

Kuhusu mafunzo alisema: “Ofisi ya Katibu Mtendaji wa Tume iendelee kuwahimiza watumishi kujiendeleza na kupata mafunzo ya muda mrefu au mfupi ili kuongeza ujuzi na maarifa katika maeneo yao ya kazi ... nawashauri kuandaa mpango endelevu wa kutoa mafunzo kwa watumishi ... kutegemeana na uwezo uliopo wa kifedha.”

Mhe. Jaji Mstaafu Mwaimu alitumia fursa hiyo pia kuhimiza kuhusu uzingatiaji wa sheria, taratibu, kanuni za maadili ya utumishi wa umma, kufanya kazi kwa bidii na uadilifu, na kutoa huduma bila upendeleo wowote.

Awali Katibu Mtendaji wa THBUB, Bwana Patience Ntwina alieleza kuwa pamoja na masuala mengine mkutano huo utapokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa majukumu ya taasisi kwa vipindi vya 2022/2023 na 2023/2024; taarifa ya makadirio ya bajeti kwa mwaka ujao wa fedha (2024/2025); na pia watajadili hoja za watumishi. Mkutano huo wa siku moja uliwashirikisha takriban wajumbe 55 kutoka makao makuu ya Ofisi za Tume Dodoma, Ofisi ya Tume Zanzibar na Ofisi za Tume za matawi ya Dar es Salaam, Lindi, Pemba na Mwanza.


Friday, February 2, 2024

THBUB kufuatilia haki za wafanyakazi katika makampuni ya ulinzi

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (katikati) akiongea na vyombo vya habari Makao Makuu ya Tume, Kilimani jijini Dodoma, leo Februari 2, 2024.
Baadhi ya Maafisa wa Tume na Waandishi wa Habari wakimsikiliza Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Mathew Mwaimu (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao leo Februari 2, 2024 Makao Makuu ya Tume Kilimani jijini Dodoma.
Baadhi ya Maafisa wa Tume na Waandishi wa Habari wakimsikiliza Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Mathew Mwaimu (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao leo Februari 2, 2024 Makao Makuu ya Tume Kilimani jijini Dodoma.


Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji Mstaafu) amesema hivi karibuni taasisi yake itafanya ufuatiliaji kuhusu utekelezaji wa haki za wafanyakazi na viwango vya ajira katika makampuni binafsi ya ulinzi.

Akiongea na vyombo vya habari Makao Makuu ya Tume, Kilimani jijini Dodoma leo Februari 2, 2024 Mhe. Mwaimu amesema kuwa ufuatiliaji huo utafanyika kuanzia Februari 5 hadi 10, 2024 katika mikoa ya Iringa, Dar es Salaam na Kagera.

“Kazi hii inalenga kufuatilia utekelezaji wa Sheria na Kanuni zinazoyataka makampuni ya aina zote kutekeleza majukumu yao kwa kuheshimu haki za binadamu na upatikanaji wa suluhisho na fidia kwa wahanga wa ukiukwaji wa haki za binadamu unaohusishwa na shughuli za kibiashara au uwekezaji,” Mhe. Jaji Mstaafu amesema.

Ameongeza kuwa miongoni mwa maeneo yatakayoangaliwa katika ufuatiliaji huo ni pamoja na: Mikataba ya ajira, iwapo inakidhi viwango vya ajira; afya na usalama kazini; na utunzaji wa taarifa binafsi za waajiriwa.

Maeneo mengine ni: Uwepo wa vyama vya wafanyakazi; mahusiano ya makampuni ya ulinzi na jamii; na stahili nyingine wanazopaswa waajiri kutoa kwa wafanyakazi wao.

Aidha, Mhe. Mwaimu amesema kuwa baada ya ufuatiliaji huo, Tume itatoa taarifa yenye mapendekezo ya namna ya kuboresha uzingatiaji wa haki za wafanyakazi na viwango vya ajira katika makampuni binafsi ya ulinzi.

Utekelezaji wa kazi hii ni mwendelezo wa ufuatiliaji wa masuala ya biashara na haki za binadamu nchini, Mhe. Mwenyekiti amesema, na kuongeza kuwa Mwezi Desemba 2023 Tume ilifanya tathimini ya utendaji kazi kwa taasisi zisizo za kimahakama zinazoshughulikia malalamiko na migogoro inayohusiana na masuala ya biashara na haki za binadamu.

“Tume inatoa shukrani zake za dhati kwa Serikali kwa kuipatia mazingira wezeshi kutekeleza majukumu yake, na kwa Taasisi ya Haki za Binadamu nchini Denmark (Danish Institute for Human Rights - DIHR) kwa kuiwezesha kiufundi na kirasilimali kufanikisha utekelezaji wa kazi hii na nyingine zilizotangulia.


Friday, January 26, 2024

Wanafunzi Chuo Kikuu cha Waislamu Moro watembelea THBUB, waipongeza

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (katikati) na Mwenyekiti wa Klabu ya haki za binadamu Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro, Bi. Asia Ashirafu (wa pili kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanachama wa Klabu hiyo na viongozi wa THBUB wanafunzi hao walipotembelea Makao Makuu ya Tume, Kilimani jijini Dodoma leo Januari 26, 2024. Wa kwanza kulia (waliokaa) ni Kiongozi wa msafara wa Klabu hiyo, Bwana Yusuf Said.
Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji Mst.), akiongea na wanachama wa Klabu ya haki za binadamu Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (hawapo pichani) leo Januari 26, 2024, wanachama hao na walimu wao walipotembelea Makao Makuu ya Tume, Kilimani jijini Dodoma. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Mohamed Khamis Hamad.
Baadhi ya wanachama wa Klabu ya haki za binadamu Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro wakipokea nasaha kutoka kwa Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji Mst.), leo Januari 26, 2024 Makao Makuu ya Tume, Kilimani jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria, THBUB, Bwana Nabor Assey akiwaeleza wanachama wa Klabu ya haki za binadamu Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro utekelezaji wa majukumu ya Tume kupitia Idara anayoiongoza, wanachama hao walipotembelea Makao Makuu ya Tume, Kilimani jijini Dodoma leo Januari 26, 2024.
Mkurugenzi wa malalamiko na uchunguzi, THBUB, Bi. Suzana Paschal akiwaeleza wanachama wa Klabu ya haki za binadamu Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro utekelezaji wa majukumu ya Tume kupitia Idara anayoiongoza, wanachama hao walipotembelea Makao Makuu ya Tume, Kilimani jijini Dodoma leo Januari 26, 2024
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (katikati) na Mwenyekiti wa Klabu ya haki za binadamu Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro, Bi. Asia Ashirafu (wa pili kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanachama wa Klabu hiyo na viongozi wa THBUB wanafunzi hao walipotembelea Makao Makuu ya Tume, Kilimani jijini Dodoma leo Januari 26, 2024. Wa kwanza kulia (waliokaa) ni Kiongozi wa msafara wa Klabu hiyo, Bwana Yusuf Said.


Wanafunzi 70 wanachama wa Klabu ya haki za binadamu Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro wakiambatana na walimu wanne (4) leo Januari 26, 2024 wametembelea Makao Makuu ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Kilimani jijini Dodoma na kujifunza masuala mbalimbali.

Wanafunzi hao wameipongeza Tume kwa juhudi zake za kulinda na kueneza elimu ya haki za binadamu na utawala bora nchini.

“Tumetembelea Tume na kujifunza masuala mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu ya Tume, tumefurahi sana, hakika mnafanya kazi nzuri iliyotukuka,” amesema mmoja wa wanafunzi hao.

“Nimefurahi pia kuwaona Mheshimiwa Mwenyekiti wa Tume na Makamishna wake, na jinsi tulivyopokelewa vizuri na kwa upendo mkubwa,” ameongeza.

Wakiwa katika ofisi hizo za Tume wanafunzi hao walipata fursa ya kuwasikiliza wakurugenzi na wakuu wa vitengo vilivyopo Tume wakielezea utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kupitia idara na vitengo wanavyosimamia. Vilevile, walipata nasaha kutoka kwa viongozi wa juu wa Tume.

Wanafunzi hao wametembelea THBUB kama taasisi ya kitaifa ya haki za binadamu na mlezi wa Klabu za haki za binadamu katika taasisi za elimu nchini, ili kujifunza namna Tume inavyotekeleza majukumu yake.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Klabu ya haki za binadamu Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro, Bi. Asia Ashirafu kila mwaka Klabu hiyo imekuwa na utaratibu wa kutembelea taasisi mbalimbali za umma kwa lengo la kujifunza kama sehemu ya masomo yao.